Kwa mujibu wa kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam Sheikh Hussein Ghabris, Afisa wa Mahusiano ya Umma wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu wa Lebanon, katika ujumbe wake uliolenga kuonesha mshikamano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema: Amani iwe juu yenu, enyi taifa la Kiislamu la Iran, huru na lenye heshima; amani iwe juu ya kiongozi wenu, alama kubwa ya Umma wa Kiislamu, marji' na mlezi wa mambo yetu, faqihi aliyekamilika kwa masharti yote, Imam na Kiongozi Sayyid Ali Khamenei – Mwenyezi Mungu amlinde. Heshima na kudumu ni za mashahidi walioungana na Ufalme wa Juu tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yenye baraka hadi leo, na wa mwisho wao ni wale waliouawa kishahidi katika siku na wiki za hivi karibuni kufuatia uchochezi wa vurugu, ghasia, mauaji na uchomaji moto.
Aliongeza kusema: Wahalifu katika matendo haya walijaribu kuvuruga utulivu wa wananchi na kudhoofisha misingi ya jamii ya Kiislamu ya Iran, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kama ilivyokuwa katika matukio kama hayo ya nyuma ambapo maadui walinuia kuidhuru, imetoka salama na kifua mbele katika mtihani huu pia.
Sheikh Ghabris alisema: Ni lazima tutoe msimamo wetu kuhusu matukio ya hivi karibuni katika baadhi ya miji ya Iran; yale yaliyofanyika kwa kisingizio cha kudai haki halali, kwa hakika hayakuwa chochote isipokuwa ghasia na uingiliaji wa makundi ya waharibifu waliounganishwa na Mossad wa Kizayuni na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA). Vipengele hivi vilivyojihami na vilivyo na mipango mahsusi, vimesababisha hasara kubwa kwa raia wasio na hatia, na hata vikosi vya usalama na polisi katika miji mbalimbali havikuokoka madhara yao.
Mjumbe wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu aliendelea kusema: Katika kukabiliana na yaliyojitokeza, pamoja na ufuatiliaji makini wa vyombo vya habari, kwanza kabisa ni lazima tutoe shukrani kwa hekima, busara na subira ya uongozi wa Jamhuri ya Kiislamu. Kwa hekima na maadili ya juu ya Kiongozi, taifa lilikusanyika pamoja na umoja wa Kiislamu ukafufuliwa tena. Taifa la waumini jasiri wa Iran, hata kabla ya wito wowote rasmi, lilijitokeza kwa mamilioni mitaani ili kutangaza kwa sauti kubwa: sisi tuko katika mstari wa Uislamu, tuko pamoja na Jamhuri ya Kiislamu yenye baraka ya Iran, hatuko pamoja na mfumo mwingine wowote, na hatutaacha mafanikio ya Mapinduzi ya Imam Khomeini (rehma za Mwenyezi Mungu zimshukie) hadi leo.
Alisisitiza kuwa: Kwa yakini kamili tunasema kuwa, Mapinduzi haya yako chini ya ulinzi na uangalizi wa Mwenyezi Mungu; Yeye anayalinda na kwa baraka ya uwepo wa Imam wa zama, Hadhrat Hujjat bin al-Hasan al-Mahdi al-Muntadhar (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake), ambaye ni hazina takatifu ya Ahlul-Bayt (a.s.), yataendelea kudumu. Kutoka hapa, Lebanon, kwa taifa la Iran ambalo tunalifahamu na tuko pamoja na mapinduzi yao, tunasema: songeni mbele kwa baraka za Mwenyezi Mungu. Tunawaombea dua na tumesimama pamoja nanyi dhidi ya maadui wenu. Kama vile tunavyolaani vikali jaribio lolote la kumvunjia heshima Imam, marejeo ya haki na Kiongozi Mkuu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei (Mwenyezi Mungu amlinde).
Sheikh Ghabris aliongeza: Maadui kupitia mashambulizi ya propaganda wanajaribu kuichafua taswira yake, lakini tumeshuhudia kuwa Waislamu duniani kote—Shia na Sunni—walijitokeza mitaani na kulaani waziwazi mashambulizi dhidi ya marjaiya ya dini.
Tunauchukulia uongozi wetu wa kidini, Ayatullah Khamenei, kama tunavyowachukulia maraaji' wengine wakubwa tunaowapenda na kuwaheshimu, kuwa ni mstari mwekundu, na tunatangaza kwamba shambulio lolote au jaribio lolote la kuidhoofisha nafasi yake ni kuvuka mipaka yote myekundu. Kutoka kwetu hamtaona chochote isipokuwa kusisitiza kuendelea na misimamo yetu na kusimama imara juu ya misingi na imani zetu. Mwenyezi Mungu amlinde Imam Khamenei, mar'aji' wengine, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mipaka yake yote ya kijiografia na ya wananchi wake. Nchi hii tukufu na yenye nguvu, kwa baraka ya elimu, maendeleo na ustaarabu wake, ni yenye heshima, na tuna yakini kuwa haitapata madhara yoyote.
Katika kuhitimisha kwake alisema: Kwa mara nyingine tena ninasisitiza kwamba; kwa mujibu wa yale yaliyoelezwa katika maarifa yetu ya ghaibu, yeyote atakayeikusudia Qom—na kusudio la Qom ni Iran yote— kwa nia mbaya, Mwenyezi Mungu atamvunja mgongo wake. Kama alivyowavunja Mafirauni wa zamani, Mwenyezi Mungu atawavunja na kuwaangamiza madhalimu wote wanaonuia uadui dhidi ya nchi hii. Ushindi na heshima ni wa Mwenyezi Mungu, Mtume wake na waja Wake waumini wema.
Maoni yako